Suzuki kufunga mtambo wa kutengeneza magari nchini Thailand

Kampuni ya Kijapani ya kutengeneza magari ya Suzuki imeamua kufunga kiwanda cha kampuni yake tanzu ya kutengeneza magari nchini Thailand ifikapo mwishoni mwa mwaka 2025.

Kampuni hiyo ilitangaza kuwa kampuni yake tanzu ya Suzuki Motor Thailand itahitimisha utengenezaji wa magari nchini humo.

Suzuki imekuwa ikitaabika na uuzaji wa magari madogo kutokana na ushindani mkali na kampuni za China za kutengeneza magari ya umeme. Kampuni hiyo pia inakabiliwa na changamoto ya kuendeleza masoko kutokana na mahitaji makubwa nchini Thailand ya magari ya ‘pickup.’

Kiwanda hicho kilianza uzalishaji nchini Thailand kuanzia mwaka 2012 na kutengeneza magari karibu 60,000 katika kipindi chake cha kuzalisha magari mengi. Hata hivyo mwaka jana, utengenezaji magari ulishuka hadi magari zaidi kidogo ya 7,000.

Kampuni hiyo ya Suzuki inasema itaendelea kuuza magari nchini Thailand, kupitia uagizaji kutoka katika viwanda vya eneo la ASEAN pamoja na Japani na India.

Hatua hiyo inafuatia tangazo la kampuni nyingine ya Kijapani ya Subaru juu ya mipango yake ya kuhitimisha utengenezaji magari nchini Thailand.