Ufaransa huenda ikatuma wakufunzi wa kijeshi nchini Ukraine

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema anataka “kuhitimisha” uundaji wa muungano wa nchi utakaopeleka wakufunzi wa kijeshi kuvifunza vikosi nchini Ukraine. Alikuwa mwenyeji wa mkutano na Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine jijini Paris jana Ijumaa na kusema kujibu ombi la Ukraine kwa wakufunzi hao haisababishi “kuongeza” migogoro na Urusi.

Macron alikabiliwa na maonyo kutoka kwa baadhi ya washirika juu ya mpango huo. Viongozi wa Marekani na Ujerumani wana wasiwasi kwamba kuwa na maafisa wa kijeshi wa nchi za Magharibi ndani ya Ukraine kunaweza kuongeza mgogoro.

Viongozi wa Urusi wanasema iwapo wakufunzi hao watapelekwa, watakuwa “walengwa halali.”

Macron pia aliahidi kutoa ndege za kivita aina ya Mirage 2000, ingawa hakutaja idadi yake. Zelenskyy alipongeza msaada huo, akisema unaonyesha kwamba “Ulaya ipo imara” zaidi ya “uovu” unaothubutu kuwatisha.