Biden amwomba radhi Zelenskyy kwa kuchelewesha msaada wa kijeshi

Rais wa Marekani Joe Biden amemwomba radhi rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy kwa ucheleweshaji wa msaada wa kijeshi wa Marekani ili kupambana na uvamizi wa Urusi.

Viongozi hao wawili walikutana jijini Paris nchini Ufaransa jana Ijumaa sambamba na matukio ya kuadhimisha miaka 80 ya D-Day.

Biden alisema Bunge la Kongresi la Marekani “lilikuwa na shida kupitisha mswada” kwa sababu “wahafidhina zaidi” walikwamisha “kuchukuliwa kwa hatua.”

Alisisitiza kwamba Wamarekani bado “wamesimama na” watu wa Ukraine na kupongeza uthabiti wao katika uvamizi wa Urusi. Kwa kiasi kikubwa Marekani ndiye msambazaji mkuu wa misaada kwa Ukraine nyakati za vita.

Biden alitumia tukio hilo kutangaza msaada wake wa sita. Ni nyongeza ya dola milioni 225 zinazojumuisha mifumo ya ulinzi wa anga na mizinga, sambamba na silaha za kupambana na vifaru.

Zelenskyy alimshukuru Biden na kuomba msaada wa Marekani kutoka vyama vyote viwili.

Alisema ni muhimu kwamba watu “wote wa Marekani wanasalia na Ukraine, kama ilivyokuwa wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia,” pale Marekani iliposaidia kuokoa maisha ya watu na Ulaya.