Vikosi vya Israel vyasema vimewaokoa mateka wanne kutoka Hamas

Vikosi vya Israel jana Jumamosi vimewaokoa mateka wanne waliokuwa wanashikiliwa na Hamas kwa kipindi cha miezi minane iliyopita, vikisema kuwa wapo katika afya nzuri.

Jeshi hilo lilisema mateka hao waliokolewa wakati wa operesheni iliyofanyika katika mji wa Nuseirat katikati mwa Ukanda wa Gaza. Lilisema mateka hao wamepelekwa hospitali nchini Israel ili kufanya vipimo vya kiafya.

Msemaji wa jeshi la Israel alisema katika mkutano na wanahabari kuwa mateka 120 bado wameshikiliwa, na kwamba litafanya juhudi za kuwaokoa.

Kabla ya kutangaza huko, vyombo vya habari nchini Palestina viliripoti kuwa jeshi la Israel lilifanya shambulizi kali kwenye mji wa Nuseirat na kwingineko. Shirika la habari la Palestina liliripoti kuwa watu wasiopungua 55 waliuawa.

Mamlaka za eneo la Gaza zililikosoa shambulizi hilo katika taarifa iliyosema jeshi la Israel lilifanya shambulizi la kinyama na kali moja kwa moja likilenga raia.