Idadi ambayo ni rekodi ya wanafunzi milioni 13.4 wafanya mitihani ya taifa ya kujiunga na vyuo

Idadi ambayo ni rekodi ya wanafunzi wa sekondari ya juu nchini China, wamefanya mitihani ya taifa ya kujiunga vyuo iliyofanywa kote nchini humo juzi Ijumaa.

Wizara ya elimu ya China inasema zaidi ya watahiniwa milioni 13.4 walijiandikisha kwa ajili ya mitihani hiyo ya siku mbili mwaka huu. Hilo ni ongezeko la wanafunzi 510,000 kutoka mwaka jana.

Visa vya udanganyifu kwenye mitihani ya taifa vimekuwa vikiripotiwa kwa miaka mingi kutokana na matokeo ya mitihani hiyo kuwa na jukumu muhimu katika maisha ya baadaye ya washiriki.

Vyombo vya habari vya China vinasema mfumo wa kupambana na udanganyifu unaotumia teknolojia ya AI umewekwa kwa mara ya kwanza kubaini tabia zisizofaa kwa watahiniwa.

Vijana wa China wanakabiliwa na ushindani mkubwa kwenye soko la ajira, na hata wahitimu wa vyuo vikuu wanahangaika kupata ajira wakati huu ukuaji uchumi ukiwa si wa uhakika.

Idadi inayoongezeka ya wanafunzi wa shule za sekondari za juu wanalenga kujiunga na vyuo na vyuo vikuu ambavyo vitawawezesha kunufaika watakapokuwa wanatafuta kuajiriwa.

Uwiano wa wanafunzi wa shule za sekondari za juu walioendelea na elimu ya vyuo vikuu au taasisi zingine za elimu ya juu imekuwa ikiongezeka. Imekua kutoka asilimia 30 mwaka 2012 hadi 60.2 mwaka jana. Matumizi ya kaya katika elimu pia yameongezeka.

Taasisi ya Takwimu ya China inasema wazazi watatumia zaidi ya dola 63,000 katika malezi ya watoto wao hadi watakapofikia umri wa miaka 17. Kiwango hicho ni pamoja na gharama za elimu.