Vyanzo: Taarifa za kina za waraka wa msaada wa Japani kwa Ukraine zaainishwa

NHK imebaini maelezo ya waraka wa pande mbili unaoainisha hatua za msaada utakaotolewa na Japani kwa Ukraine. Vyanzo vinasema serikali ya Japani inapanga kusaini waraka na Ukraine pembezoni mwa mkutano wa juma lijalo wa viongozi wakuu wa Kundi la Nchi Saba Zilizostawi Zaidi Kiviwanda Duniani G7.

Mipango inaripotiwa kuendelea kwa Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenkskyy kufanya mazungumzo na kusaini waraka pembezoni mwa mkutano wa viongozi wakuu wa G7 nchini Italia kuanzia Juni 13.

NHK imebaini kwamba waraka huo umepangwa kusema kuwa Japani itaendelea kutoa msaada wa usalama na ulinzi kwa Ukraine ndani ya mfumo wa Katiba ya nchi hiyo.

Hatua hizo zitajumuisha usambazaji wa vifaa visivyo vya kivita, kutibu wanajeshi wa Ukraine waliojeruhiwa na ushirikiano katika nyanja ya intelijensia.

Kwa upande wa ujenzi mpya, waraka huo unatarajiwa kusema kwamba Japani itatoa msaada katika kuondoa mabomu yaliyotegwa ardhini, kuboresha hali ya ubinadamu kwa wanawake na watoto na kujenga tena maisha yao, na kuendeleza sekta ya kilimo.

Waraka huo utakuwa halali kwa miaka 10 na kuthibitisha Japani kuendelea kuisaidia Ukraine.