Wanaanga wa Marekani ndani ya chombo cha Boeing Starliner wawasili ISS

Wanaanga wawili wa Marekani wamewasili kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu, ISS baada ya kutua kwenye kituo hicho kinachoizunguka dunia kwa kutumia chombo chao cha anga za juu cha Boeing Starliner.

Sunita Williams na Barry “Butch” Wilmore walisafiri kwa zaidi ya saa 24 baada ya kuruka juzi Jumatano kwenda kuungana na wanaanga wengine saba walioko ISS. Wanaanga hao saba waliwasili kwenye kituo hicho wakiwa kwenye chombo cha Dragon cha kampuni ya SpaceX au chombo cha Soyuz cha Urusi.

Williams na Wilmore wanatarajiwa kusalia kwenye kituo hicho kwa takribani juma moja kabla ya kutumia chombo cha Starliner kurejea kwenye Dunia. Kampuni ya Boeing inasema timu yake “imelenga” kuwarejesha wawili hao duniani wakiwa salama.

Shirika la Anga za Juu la NASA limekuwa likishirikiana na kampuni za kibinafsi kutafuta njia zenye “gharama nafuu” za kuwasafirisha wanaanga. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, NASA imetegemea chombo cha Dragon, lakini chombo cha Starliner kinaipatia chaguo lingine. Maafisa wanasema kuwa na vyombo viwili vilivyotengenezwa nchini Marekani kunatoa “usaidizi” salama.