Wanajeshi wastaafu, viongozi wa dunia waadhimisha miaka 80 ya D-Day

Wanajeshi wastaafu wa vikosi vya Muungano vilivyovamia fukwe za Normandy miaka 80 iliyopita wamerejea nchini Ufaransa kuadhmisha Siku ya Uvamizi wa Vikosi vya Muungano, yaani D-Day. Viongozi wa dunia waliungana nao wakati wa maadhimisho ya siku ya mapambano hayo muhimu ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Wanajeshi zaidi ya 150,000 walitua kwenye fukwe tano Juni 6, 1944 kuvifurusha vikosi vya Ujerumani ya Kinazi.

Idadi inayopungua ya wanajeshi ambao bado wako hai waliwaenzi wale waliofariki, wakiwa pamoja na viongozi wa nchi Muungano na Ujerumani. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy pia alihudhuria, akielezea uhusiano wa siku zilizopita na za sasa.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema, “Tukikabiliwa na wale wanaodai kubadilisha mipaka kwa nguvu na kuandika upya historia, hebu tuwe wa thamani kwa wale waliotua hapa.” Aliongeza kuwa uwepo wa Zelenskyy kwenye hafla hiyo “unaelezea yote.”

Wanajeshi wastaafu wa Marekani walikusanyika kwenye Makaburi ya Marekani na kusikiliza wakati Rais Joe Biden akionya juu ya hatari za kuwainamia madikteta.

Biden alisema: “Ikiwa tutafanya hivyo, inamaanisha tutakuwa tunasahahu kilichofanyika hapa katika fukwe hizi takatifu. Usidanganywe: Hatutawainamia.”