Kikosi cha Ulinzi wa Pwani cha Japani kinaangazia kuunda meli yake kubwa zaidi ya doria

NHK imegundua kuwa maafisa wa Walinzi wa Pwani wa Japani wanaangazia kuunda meli mpya ya doria ambayo ni kubwa zaidi kuliko yoyote waliyowahi kuwa nayo.

Vyanzo vilivyo karibu na suala hilo vinasema kuwa meli hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba makumi ya boti zenye kasi zilizoundwa kwa mpira, pamoja na helikopta tatu.

Wanasema meli hiyo inatarajiwa kujumuisha uwezo wa kuamuru meli zingine za doria, ikitumika kama kambi ya baharini wakati wa misheni.

Vyanzo vya habari vinasema maafisa wa Walinzi wa Pwani wanafikiria kutumia meli hiyo kwa operesheni karibu na Visiwa vya Senkaku katika Bahari ya China Mashariki, kwa kusafirisha wakaazi katika hali ya dharura, na shughuli za kukabiliana na majanga, miongoni mwa misheni zingine.

Wanasema meli hiyo inatarajiwa kuwa na boti nyingi zilizoundwa kwa mpira endapo itahitaji kukabiliana na idadi kubwa ya meli kuliko meli za doria za Walinzi wa Pwani wakati wa misheni.

Vyanzo vy habari vinasema maafisa wa Walinzi wa Pwani pia wanafikiria kuunda meli hiyo ili kubeba hadi abiria 1,500, pamoja na makontena.

Wanasema Walinzi wa Pwani wanalenga kuweka meli hiyo katika matumizi wakati fulani katika mwaka wa fedha 2029, na kuna mpango wa kuongeza meli ya aina hiyo katika siku zijazo.