Israeli yatetea shambulio katika shule huku ikiendeleza mashambulizi Ukanda wa Gaza

Jana Ijumaa ilitimia miezi nane tangu mapigano yalipoibuka kati ya Israeli na Hamas katika Ukanda wa Gaza. Vikosi vya Israeli vinaendelea kufanya operesheni kali huko, ingawa wamekosolewa kwa kutekeleza shambulizi kwenye shule ya Umoja wa Mataifa UN lililosababisha vifo vya watu 40.

Jeshi lilisema juzi Alhamisi kwamba lilifanya shambulio la anga kwenye shule katika eneo la Nuseirat, ambalo lipo katikati mwa Ukanda wa Gaza. Shule hiyo inaendeshwa Shirika la UN la Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA. Maafisa wa afya katika Ukanda wa Gaza wanasema shambulio hilo lilisababisha vifo vya watu 40 wakiwemo watoto 14. Pia linasema kwamba watu wengine 74 walijeruhiwa.

Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres alilaani shambulio hilo. Alisema kuwa majengo ya UN hayakiukwi na lazima yalindwe na pande zote wakati wote.

Juzi Alhamisi, msemaji wa jeshi la Israeli, Daniel Hagari alitetea shambulizi hilo la anga. Alisema kwamba wapiganaji wa kundi la Hamas na wengine walikuwa wakiendesha operesheni ndani ya madarasa matatu kwenye shule hiyo ya UN.

Hagari alisema, "Tulifanya shambulizi hilo mara tu taarifa zetu za kijasusi na uchunguzi zilipoonyesha kuwa hakuna wanawake na watoto ndani ya eneo la Hamas, ndani ya vyumba hivyo vya madarasa." Pia alionyesha picha za watu kadhaa aliowaita magaidi. Hagari alidai kuwa watu hao waliuawa katika shambulio hilo.

Vikosi vya Israeli viliendelea kutekeleza mashambulizi makali katika eneo la Nuseirat na maeneo yake ya karibu jana Ijumaa. Shirika la habari katika eneo hilo linasema zaidi ya watu 10 waliuawa.