Kundi la Indo-Pasifiki lakubaliana juu ya malengo ya uchumi safi na wenye usawa

Kundi la nchi kadhaa lililoundwa kukabiliana na kuongezeka kwa ushawishi wa China barani Asia lilikubaliana jana Alhamisi kukuza uwekezaji katika kupunguza uzalishaji wa kaboni na kulenga usawa wa kiuchumi.

Mawaziri kutoka nchi 14 za Mpangokazi wa Kiuchumi wa Indo-Pasifiki kwa ajili ya Ustawi walisaini taarifa zinazoweka malengo ya chumi safi na zenye usawa katika eneo hilo.

Nchi wanachama zikiwemo Japani, Marekani na India zilifikia makubaliano juu ya malengo hayo mwezi Novemba mwaka 2023.

Makubaliano ya uchumi safi yanalenga uwekezaji wa nchi wanachama wa dola zisizopungua bilioni 120 katika nishati mbadala na hifadhi ya umeme.

Makubaliano ya “uchumi wenye usawa” yanaweka lengo la kuzuia ufisadi.

Awali, nchi wanachama zilitia saini makubaliano ya kulinda mitungo ya usambazaji wa nyenzo muhimu katika eneo hilo.

Kundi hilo limesema pia litatafuta makubaliano katika biashara.

Uwezekano wa kufanyika kwa mazungumzo juu ya makubaliano kama hayo ya kibiashara huenda ukategemea matokeo ya uchaguzi wa urais nchini Marekani uliopangwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu.