Biden: Ukraine haijaruhusiwa kutumia silaha za Marekani kushambulia mji wa Moscow

Rais wa Marekani Joe Biden jana Alhamisi katika mahojiano na televisheni ya ABC alisema kuwa silaha za Marekani zinaruhusiwa kutumika ndani ya Urusi katika maeneo yaliyopo karibu na mpaka kati ya nchi hiyo na Ukraine. Alisema, “Marekani hairuhusu mashambulizi mjini Moscow, kwenye Ikulu.”

Hivi karibuni, Biden aliiruhusu Ukraine kutumia silaha za Marekani kushambulia vikosi vya Urusi vilivyopo kwenye upande wake wa mpaka.

Awali, Marekani iliiruhusu tu Ukraine kutumia silaha zilizotolewa na Marekani dhidi ya vikosi vya Urusi ndani ya Ukraine. Mabadiliko katika sera ya Marekani yamekuja baada ya Urusi kuzidisha mashambulizi yake hasa katika eneo la mashariki la Kharkiv.

Inaonekana Biden anatumai kuepuka kuzidisha mivutano na Urusi kwa kusisitiza kuwa, mashambulizi kwa kutumia silaha za Marekani ndani ya Urusi yataruhusiwa tu katika maeneo yaliyopo karibu na mpaka.