Baraza Kuu la UN lamchagua kiongozi wa zamani wa Cameroon kuwa Rais mpya

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limemchagua Waziri Mkuu wa zamani wa Cameroon Philemon Yang kuwa Rais ajaye wa baraza hilo. Muhula wake wa mwaka mmoja utaanza mwezi Septemba mwaka huu.

Katika hotuba jana Alhamisi, Yang alisema mivutano ya siasa za kimaeneo inaendelea kuchochea hali ya kutoaminiana miongoni mwa mataifa na kuzidisha mashindano ya silaha. Aliongeza kusema kwamba migogoro inaongezeka katika maeneo mbalimbali duniani ikisababisha vifo vingi vya raia, na “visa vya Gaza na Ukraine ni mifano inayoumiza zaidi inayoelezea hali hiyo.”

Baraza hilo pia lilizichagua nchi tano zisizokuwa wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama kwa muhula wa miaka miwili kuanzia mwezi Januari mwaka 2025. Nchi za Dernmark, Ugiriki, Pakistan, Panama na Somalia zilichaguliwa kutoka kwa wagombea wanaowakilisha kila eneo duniani.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pamoja na Baraza la Usalama yanaendelea kutafuta njia za kushughulikia makabiliano na tofauti zinazoongezeka kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na mapigano kati ya Israel na Hamas.