Japani kuimarisha ushirikano na Ukraine kusaidia ujenzi mpya wa nchi hiyo

Serikali ya Japani inafanya kazi kusaini waraka mpya na Ukraine ambao unajumuisha hatua za kiuchumi za kusaidia ujenzi mpya wa nchi hiyo.

Vyanzo vya habari serikalini vinasema mipango inaendelea ya Waziri Mkuu Kishida Fumio na Rais Volodymyr Zelenskyy kufanya mazungumzo na kusaini waraka huo pembezoni mwa mkutano wa mwaka huu wa viongozi wakuu wa Kundi la Nchi Saba zilizostawi zaidi kiviwanda duniani - G7. Mkutano huo utafanyika nchini Italia kuanzia Juni 13. Zelenskyy amealikwa kuhudhiria kikao kinachoangazia hali nchini Ukraine.

Ukraine imekamilisha makubaliano juu ya ushirikiano wa kiusalama na nchi kama vile Uingereza na Ufaransa.

Vyanzo vya habari katika serikali ya Japani vinasema kutokana na vizuizi vya Kikatiba kwa upande wa nchi hiyo miongoni mwa vigezo vingine, ushirikiano unaotazamiwa huenda ukajikita kwenye usaidizi wa kiuchumi ili kusaidia kuijenga upya Ukraine huku angalizo likitolewa kwa sekta ya nishati.