Israel yashambulia shule ya UN eneo la Gaza mkesha wa maadhimisho ya miezi 8 tangu kuanza kwa mgogoro

Israel inasema imefanya shambulizi la anga kwenye shule ya Umoja wa Mataifa, UN katikati mwa Ukanda wa Gaza. Maafisa wa afya katika ukanda huo wanasema shambulizi hilo limeua watu 40, wakiwemo watoto 14 na wanawake tisa.

Jeshi la Israel lilitangaza kufanywa kwa shambulizi hilo jana Alhamisi, mkesha wa maadhimisho ya miezi minane tangu kuanza kwa mgogoro unaoendelea kati ya Israel na Hamas huko Gaza.

Jeshi hilo lilisema ndege zake za kivita “zilifanya shambulizi mahsusi kwenye ua wa Hamas uliopo ndani” ya shule ya shirika la UN linalowashughulikia wakimbizi Wapalestina, UNRWA katika eneo la Nuseirat.

Aidha Jeshi hilo liliongeza kuwa shambulizi hilo limeua wapiganaji wengi wa Hamas kwenye ua huo. Lilisisitiza kwamba “hatua kadhaa” zilichukuliwa ili kupunguza hatari ya kuwadhuru raia wasiohusika wakati wa shambulizi hilo.

Kamishna Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini alishutumu shambulizi hilo kwenye ujumbe alioweka katika mitandao ya kijamii, akisema shule hiyo ilikuwa ikihifadhi watu 6,000 waliopoteza makazi iliposhambuliwa.

Maafisa wa afya katika eneo la Gaza wanasema idadi ya wagonjwa na waliojeruhiwa wanaohitaji kusafirishwa kwa ajili ya matibabu nje ya eneo hilo imefikia 25,000. Lakini maafisa wanasema hakuna miongoni mwao aliyeweza kuondoka eneo la Gaza kwa sababu jeshi la Israel mwezi uliopita lilidhibiti mpaka wa Rafah kati ya eneo hilo na Misri.