Putin afungua kongamano la kiuchumi la kila mwaka, St. Petersburg

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema anataka kupanua ushirikiano wa kiuchumi katika kile alichokiita “dunia yenye mataifa mengi yenye nguvu.” Putin alifungua Kongamano la Kimataifa la Kiuchumi jana Jumatano, ambalo hufanyika kila mwaka.

Waandaaji wanatarajia kuwakaribisha washiriki 17,000 kutoka nchi na maeneo 136 wiki hii yote. Mwaka huu wanaangazia kuimarisha uhusiano na India, China na nchi zingine katika mpangokazi wa BRICS.

Uchumi wa Urusi umeyumbishwa na vikwazo vya nchi za magharibi tangu uvamizi wake nchini Ukraine miaka miwili iliyopita, lakini Putin amesema ukuaji katika robo mwaka ya kwanza 2024 umefika asilimia 5.4.

Mabinti wa Putin pia wanashiriki kwenye kongamano hilo. Katerina Tikhonova ambaye ni mtendaji wa biashara, atashiriki katika kikao cha sekta ya ulinzi; Maria Vorontsova, mtaalam wa utafiti wa kijenetiki, atazungumzia uhusiano kati ya biolojia na uchumi. Wote wamewekewa vikwazo, ikiwemo kushikiliwa kwa mali zao na marufuku ya kusafiri.

Aidha Putin pia amelialika kundi lingine lililo chini ya adhabu za kiuchumi. Anatarajiwa kuiondoa Taliban kwenye orodha ya makundi ya kigaidi yaliyopigwa marufuku na kuwatambua viongozi wake kama “utawala” halali nchini Afghanistan.