Waziri Mkuu wa Japani atoa wito wa kupitishwa kwa mswada wa mpango mpya wa mafunzo ya wafanyakazi wa kigeni

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio amerejelea wito wake kwa wabunge kupitisha mswada wa serikali utakaotambulisha mpango mpya wa kukuza ujuzi wa wafanyakazi wa kigeni ili kusaidia kupunguza uhaba wa wafanyakazi nchini humo.

Kishida alizungumza hayo kwenye Kamati ya Masuala ya Kisheria ya Baraza la Juu la Bunge jana Alhamisi. Alisisitiza umuhimu wa kuanzisha jamii jumuishi ambapo raia wa kigeni watafanya kazi kwa kutumia kikamilifu uwezo wao.

Alisema ni muhimu kupata wafanyakazi wa kigeni wenye vipaji nchini Japani wakati ushindani unaongezeka miongoni mwa nchi ili kuwavutia.

Muswada huo uliopendekezwa utafanyia mapitio sheria ya uhamiaji na sheria zingine husika.

Mapitio hayo yatachukua nafasi ya mpango wa sasa wa mafunzo ya wanagenzi wa kiufundi kwa raia wa kigeni kwa kuweka mfumo mpya wa kuwapatia mafunzo ili kupunguza uhaba wa wafanyakazi katika sekta kadhaa kama vile huduma ya uangalizi wa wazee na ujenzi.

Mpango huo mpya huenda ukaongeza idadi ya raia wa kigeni wenye hadhi ya ukazi wa kudumu. Lakini hoja moja lenye utata ni kwamba mswada huo uliopendekezwa unaweza ukaruhusu serikali kufuta hadhi ya ukazi wa kudumu chini ya hali fulani. Hilo linaweza kufanyika mathalani iwapo raia wa kigeni wameshindwa kwa makusudi kulipa kodi.

Katika kikao cha kamati hiyo, mbunge wa chama cha upinzani cha Constitutional Democratic alisema nyingi ya hoja muhimu zimeelezewa kwa maneno yasiyoeleweka yanayoacha nafasi kubwa ya kutafsiriwa.

Kishida alijibu kwamba serikali inapanga kuandaa seti ya miongozo ya kesi za kawaida za kubatilisha hadhi ya ukazi wa kudumu.