Nvidia yawa kampuni ya pili kwa kuwa na thamani kubwa zaidi duniani

Kampuni ya pili kwa thamani zaidi duniani baada ya Microsoft kwa sasa ni Nvidia. Kampuni hiyo kubwa ya semikondakta ya nchini Marekani iliipiku Apple kufuatia kuongezeka kwa mahitaji ya chipu za akili mnemba AI.

Bei ya hisa za Nvidia ilipanda kwa zaidi ya asilimia tano jana Jumatano kwenye soko la hisa za kampuni za teknolojia, Nasdaq. Ilihitimisha siku kwa bei ya hisa ya dola 1,224. Thamani ya kampuni ilizidi dola trilioni 3 kwa mara ya kwanza.

Ni kampuni ya tatu kupita alama hiyo baada ya Apple na Microsoft. Faida halisi ya Nvidia ilipanda zaidi ya mara saba kwa mwaka katika kipindi cha robo mwaka ya hadi mwezi Aprili.