Mwanamume mwenye uraia Ukraine-Urusi akamatwa nchini Ufaransa kwa tuhuma za ugaidi

Mamlaka nchini Ufaransa imemkamata mwanamume mmoja mwenye uraia wa Ukraine-Urusi kwa tuhuma za ugaidi kwa madai ya kujaribu kutengeneza kilipuzi kwenye chumba cha hoteli.

Ufaransa imekuwa katika hali ya tahadhari katika maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Paris, itakayofunguliwa mwezi ujao.

Waendesha mashtaka wa Ufaransa wanasema kuwa raia huyo mwenye umri wa miaka 26 aliungua vibaya kutokana na mlipuko katika chumba cha hoteli nje ya Paris Jumatatu iliyopita.

Wachunguzi walipata vifaa vilivyotumika kutengenezea vilipuzi katika eneo la tukio.

Walimkamata mtu huyo kwa tuhuma za kushiriki katika njama ya ugaidi na kutega bomu.

Baadhi ya vyombo vya habari vya Ufaransa vimeripoti kuwa mwanamume huyo anatoka mashariki mwa Ukraine

Vimenukuu vyanzo vya uchunguzi vikisema alikuwa akipigana upande wa Urusi katika uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.