Zelenskyy aashiria mwezi Juni, wenye mfululizo wa mikutano, kuwa mwezi muhimu

Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine anatarajiwa kuzuru nchini Ufaransa kwa ajili ya mazungumzo tofauti na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Raias wa Marekani Joe Biden.

Zelenskyy anatarajiwa kuhudhuria tukio leo Alhamisi la kuadhimisha miaka 80 ya uvamizi wa vikosi vya muungano huko kaskazini mwa Ufaransa uliosaidia kumaliza Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Ofisi ya Rais wa Ufaransa imesema Macron na Zelenskyy watafanya mazungumzo jijini Paris kesho Ijumaa.

Vyombo kadhaa vya habari vimeripoti juu ya uwezekano kwamba Ufaransa itaainisha mipango ya kupeleka wakufunzi wa kijeshi nchini Ukraine.

Wakati huo huo, Italia itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Viongozi Wakuu wa Nchi Saba zilizostawi zaidi kiviwanda duniani kuanzia Juni 13, huku Uswizi ikiandaa mkutano wa kimataifa wa kuendeleza mchakato wa amani kwa Ukraine, uliopendekezwa na Zelenskyy, kuanzia Juni 15.

Katika hotuba yake kwa njia ya video juzi Jumanne, Zelenskyy alisema, “Ni mwanzo tu wa mwezi Juni, lakini tayari haya ni majuma ambayo yataamua hali ya msimu wote wa joto na, kwa njia nyingi, mwaka huu.”

Kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov, akiwa ziarani barani Afrika, alifanya mazungumzo na mwenzake wa Jamhuri ya Kongo juzi Jumanne.

Lavrov alipuuza umuhimu wa mkutano wa Uswizi, akisema si Rais wa Jamhuri ya Kongo wala viongozi wa China, India, Brazil au Afrika Kusini wanaoamini kwamba mazungumzo bila ushiriki wa Urusi yana maana.