WMO inaona kuna uwezekano wa 80% wa joto duniani kuzidi kiwango cha nyuzi 1.5

Shirika la Hali ya Hewa Duniani, WMO linasema kuna uwezekano wa asilimia 80 ndani ya miaka mitano kwamba wastani wa halijoto duniani utazidi "kwa muda" nyuzi 1.5 za selisiasi juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda.

Jana Jumatano, shirika hilo la Umoja wa Mataifa lilichapisha matokeo ya uchambuzi wa hali ya hewa duniani na utabiri wa kati ya 2024 na 2028 kulingana na data kutoka kwa mamlaka za hali ya hewa duniani kote.

Ripoti hiyo inatabiri kuwa wastani wa halijoto karibu na uso wa dunia kwa kila mwaka katika miaka hiyo mitano utakuwa kati ya nyuzi 1.1 hadi 1.9 kikiwa juu zaidi ya wastani wa miaka kuanzia 1850 hadi 1900.

Pia ripoti hiyo inasema kuna uwezekano wa asilimia 86 kwamba walau mwaka mmoja utaweka rekodi mpya ya halijoto, ikiishinda ile ya mwaka 2023, takwimu ilipokuwa nyuzi 1.45 juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda.

Wanachama katika Mkataba wa Paris wa 2015 wanalenga kuweka ukomo kwa ongezeko la wastani wa joto hadi nyuzi 1.5.

Naibu Katibu Mkuu wa WMO Ko Barrett amesema, "Nyuma ya takwimu hizi kuna ukweli unaohuzunisha kwamba tuko mbali sana kufikia malengo yaliyowekwa katika Mkataba wa Paris."