TSMC ya Taiwan huenda ikajenga mtambo wa tatu wa sakiti changamano nchini Japani

Mkuu wa kampuni kubwa duniani ya kutengeneza sakiti changamano amesema kampuni hiyo inafikiria mipango ya kujenga mtambo wa tatu wa kutengeneza sakiti hizo nchini Japani.

C. C. Wei, ambaye ni afisa mkuu mtendaji wa Taiwan Semiconductor Manufacturing Company (TSMC), aliwaambia wanahabari kuwa kampuni hiyo inafanya utafiti zaidi juu ya upanuzi nchini Japani.

Alitoa maoni hayo baada ya kikao cha wamiliki wa hisa wa TSMC kilichofanyika jana Jumanne. Katika kikao cha bodi kilichofanyika baadaye jana Jumanne, Wei pia aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa TSMC.

Wei anasema kampuni hiyo imekuwa ikiombwa na mamlaka za maeneo za Japani kujenga mtambo wa tatu, akiongeza kuwa hilo pia litahitaji idhini kutoka kwa wakazi wa maeneo husika.