Biden asema haondoi matumzi ya nguvu ikiwa China itaivamia Taiwan

Rais wa Marekani Joe Biden amesema haondoi uwezekano wa kutumia nguvu ya vikosi vya kijeshi ikiwa China itaivamia Taiwan.

Biden ametoa maoni hayo wakati wa mahojiano na jarida la Time katika Ikulu ya Marekani mnamo Mei 28. Jarida hilo lilitoa maudhui ya mahojiano hayo jana Jumanne.

Biden alisema ameweka wazi kwa Rais wa China Xi Jinping kuwa Marekani haitafuti uhuru wa Taiwan. Alisema kuwa hiyo ndio sera ya muda mrefu ya Marekani.

Lakini alisema haondoi matumizi ya vikosi vya Marekani katika tukio la uvamizi. Awali rais huyo aligusia kuwa inawezekana jeshi la Marekani litailinda Taiwan, ikiwa China itajaribu kuleta muungano na Taiwan kwa kutumia nguvu.

Alipoulizwa iwapo jeshi la Marekani litaanzisha mashambulizi kutoka katika kambi zake nchini Japani ama Ufilipino, Biden alisema, “siwezi kuzungumzia hilo.”