Watu 4 wamekamatwa Hong Kong katika kumbukumbu ya miaka 35 ya ukandamizaji katika Uwanja wa Tiananmen

Mamlaka ya Hong Kong imewakamata watu wanne katika maadhimisho ya miaka 35 ya ukandamizaji wa umwagaji damu dhidi ya maandamano ya kuunga mkono demokrasia yaliyotokea katika uwanja wa Tiananmen jijini Beijing, nchini China.

Ukamataji huo ulifanyika jana Jumanne. Ulinzi ulikuwa mkali katika maeneo karibu na bustani ambapo watu huko Hong Kong walikuwa wakikusanyika kwa mikesha ya tarehe 4 Juni kila mwaka. Tukio hilo halijafanyika tangu mwaka 2019, kwa sababu ya ukandamizaji wa serikali.

Maafisa wa polisi huko Hong Kong wanasema waliwakamata watu wanne wenye umri wa kati ya miaka 23 na 69. Wanasema mwanamke mwenye umri wa miaka 68 aliwekwa kizuizini kwa tuhuma za kukiuka sheria mpya ya usalama wa taifa ya Hong Kong, iliyoanza kutekelezwa mwezi Machi. Wanasema alitoa kauli mbiu barabarani kwa nia ya kuchochea chuki dhidi ya mamlaka, ikiwa ni pamoja na serikali ya China.

Mamlaka pia ilisafirisha watu wengine watano, akiwemo raia mmoja wa Japani, kwenda kwenye idara ya polisi. Lakini inasemekana baadaye waliwaachilia watu hao.