Muungano wa Modi umeshinda kwa wingi wa viti katika uchaguzi wa India, lakini chama chake kimepoteza viti

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ametangaza ushindi katika uchaguzi mkuu nchini humo huku muungano wake unaoongozwa na chama tawala ukiendelea kuwa na viti vingi. Lakini chama chake kilishindwa kupata wingi wa viti wa chama kimoja.

Shughuli ya kuhesabu kura ilianza jana Jumanne. Uchaguzi huo ulianza mwezi Aprili, kukiwa na viti 543 katika baraza la chini la Bunge la India.

Matokeo yaliyotolewa na Tume ya Uchaguzi mapema leo Jumatano yalionesha kwamba muungano wa Modi unaoongozwa na Chama cha Bharatiya Janata, au BJP ulipata viti 293.

Muungano huo wa vyama tawala huenda ukaharakisha kufanya mazungumzo ili kuendeleza utawala wa Modi kwa muhula wa tatu. Lakini chama chake cha BJP kilipunguzwa hadi kufikia viti 240.

Wachambuzi wanaeleza kuwa wapiga kura, hasa katika maeneo ya vijijini, hawaridhishwi na kuongezeka kwa tofauti za kiuchumi na ukosefu mkubwa wa ajira licha ya ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo chini ya uongozi wa Modi.