Ukraine yafurahia idhinisho kubwa la kutumia silaha za mataifa ya Magharibi kushambulia ndani ya Urusi

Waziri wa ulinzi wa Uholanzi, Kajsa Ollongren, amesema kuwa nchi yake inadhamiria kuiruhusu Ukraine kushambulia maeneo lengwa ndani ya Urusi kwa kutumia silaha za Uholanzi.

Ollongren alisema hayo katika mahojiano yaliyotolewa juzi Jumatatu kwenye tovuti ya habari za kisiasa ya Marekani ya Politico.

Waziri huyo wa ulinzi alizungumzia ndege za kijeshi 24 za F-16 ambazo nchi yake inadhamiria kuziwasilisha nchini Ukraine. Alisema, “Mara tutakapokabidhi kwa Ukraine, ni za kwao kutumia.”

Ollongren alisema Uholanzi inaiomba Ukraine kutii tu sheria za kimataifa na haki ya kujilinda. Aliongeza kuwa ina maana Ukraine inaweza kutumia ndege hizo kushambulia maeneo lengwa ya kijeshi kwa ajili ya kujilinda.

Hatua yake inakuja wakati Marekani na Ujerumani zikitangaza kuwa watabadili sera zao na kuiruhusu Ukraine kushambulia ndani ya Urusi kwa silaha zilizotolewa na nchi zao katika juhudi za kuimarisha ulinzi wa eneo la Kharkiv lililopo mashariki mwa Ukraine.