Netanyahu: Makubaliano ya kusitisha vita ‘hayajakamilika’

Vyombo vya habari nchini Israel vimemnukuu Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akisema madai yanayoashiria serikali yake imekubali makubaliano ya kusitisha vita yaliyowasilishwa na Rais wa Marekani Joe Biden “si sahihi.” Netanyahu alizungumza na wabunge jijini Jerusalem jana Jumatatu kwenye mkutano wa faragha wa kamati ya serikali ya masuala ya kigeni na ulinzi.

Ijumaa iliyopita, Biden alifichua mpango unaojumuisha usitishaji wa vita, kuondolewa kwa vikosi vya Israel katika eneo la Gaza na kurejeshwa kwa mateka wote wanaoshikiliwa na Hamas. Ripoti za vyombo vya habari zimemnukuu Netanyahu akisema kwamba pendekezo hilo “halijakamilika.”

Netanyahu amesema kuna “mapengo” kati ya kile anachokizungumzia kuhusu mpango huo na Biden anavyouzungumzia. Amesema Israel imedumisha “malengo” yake ya vita hivyo, ambayo kimsingi ni “kuitokomeza Hamas.”

Vyombo vya habari nchini Lebanon vimewanukuu viongozi wa Hamas wakisema wanataka kuona “makubaliano ya maandishi.” Wamesema hawawezi kutegemea kauli za Biden na hawawezi kutia saini makubaliano ambayo “hayahakikishi usitishaji vita wa kudumu.”

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Matthew Miller jana Jumatatu alisema kuwa pendekezo hilo liliwasilishwa kwa Hamas lakini hakujakuwa na mwitikio wowote. Alisema Marekani “ina uhakika kabisa” kuwa Israel inakubali masharti ya makubaliano hayo.