Japani yawasilisha wasiwasi kwa China juu ya uchoraji kwenye nguzo katika Hekalu la Yasukuni

Japani imewasilisha wasiwasi wake kwa China juu ya raia wa China anayeshukiwa kuchora kwenye nguzo ya mawe kwa kupulizia rangi katika Hekalu la Yasukuni lililopo jijini Tokyo.

Hekalu hilo huwakumbuka waliokufa vitani nchini Japani. Wale wanaokumbukwa ni pamoja na viongozi wa wahalifu wa kivita waliotiwa hatiani baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Japani Kamikawa Yoko alisema kwenye mkutano na wanahabari jana Jumanne kuwa wizara hiyo imewasilisha wasiwasi wake kwa serikali ya China kupitia njia za kidiplomasia.

Uchoraji huo wa rangi nyekundu ulibainika Jumamosi iliyopita. Picha ya video iliyotumwa kwenye mtandao wa kijamii wa China ilionesha mwanaume mmoja akipulizia rangi kwenye nguzo. Polisi jijini Tokyo inamshuku raia wa China katika picha hiyo ya video kuwa anahusika katika uchoraji huo wa kwenye nguzo na inafanya uchunguzi.

Kamikawa alisema haikubaliki kutengeneza na kusambaza picha ya video ambayo inathibitisha na kuhamasisha kitendo kama hicho.

Aliongeza kuwa alitoa wito kwa serikali ya China kuwasihi raia wake kutii sheria na kanuni na kuwa watulivu.