Korea Kusini yaamua rasmi kusitisha makubaliano ya kijeshi na Korea Kaskazini

Serikali ya Korea Kusini imeamua rasmi kusitisha kabisa makubaliano ya kijeshi yaliyobuniwa ili kupunguza hali ya wasiwasi na Korea Kaskazini. Makubaliano hayo yalisainiwa na utawala uliopita wa Korea Kusini mwaka 2018.

Katika kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika jana Jumanne, serikali hiyo iliamua kusitisha makubaliano hayo hadi hali ya uaminifu ya pamoja itakaporejeshwa. Baadaye Rais Yoon Suk-yeol aliidhinisha uamuzi huo.

Hatua hiyo inafuatia vitendo vya kichokozi vya Korea Kaskazini vilivyofanywa hivi karibuni. Nchi hiyo imetuma idadi kubwa ya maputo yaliyojaa taka na kinyesi nchini Korea Kusini na kujaribu kukwamisha mawimbi ya GPS katika Bahari ya Njano nje kidogo ya pwani ya magharibi ya Rasi ya Korea tangu mwishoni mwa mwezi uliopita.

Vyanzo vya habari vya wizara ya ulinzi ya Korea Kusini vinasema nchi hiyo inapanga kurejesha mazoezi ya kijeshi karibu na mpaka unaotenganisha nchi hizo mbili za Korea na maeneo karibu na visiwa.