Wahandisi wa Japani watengeneza satelaiti ya mbao ya kwanza duniani

Wahandisi nchini Japani wametengeneza satelaiti ya mbao ya kwanza duniani. Wahandisi hao wanatumai kuthibitisha kuwa mbao inaweza kutumika katika anga za juu.

Chuo Kikuu cha Kyoto na kampuni ya kutengeneza nyumba ya Sumitomo Forestry kwa pamoja zilitengeneza satelaiti hiyo, yenye ukubwa wa sentimita 10 za ujazo kwa mbao zilizofunika pande zote sita.

Satelaiti nyingi zinabuniwa ili kuungua mara zinapoingia tena kwenye angahewa.

Lakini satelaiti za kisasa zinazotengenezwa na chuma zinaweza kutengeneza chembe chembe zinapoingia tena kwenye angahewa ambazo zinaathiri hali ya hewa na mfumo wa mawasiliano. Kwa kutumia mbao athari hizo zinaweza kupunguzwa.

Mwanaanga na Profesa wa Chuo Kikuu cha Kyoto Doi Takao anasema wanatumai kuthibitisha kuwa mbao ni nyenzo imara katika anga za juu, kwa sababu wakati satelaiti nyingi zikiwa zinarushwa, madhara yake hayawezi kupuuzwa.