Utengenezaji na usafirishaji wa magari wasitishwa baada ya kashfa ya majaribio ya usalama

Kampuni mbili kati ya tano za Kijapani zilizohusika katika kashfa za majaribio ya usalama wa magari zinasema zitasitisha utengenezaji wa aina za magari yaliyoathirika.

Kampuni ya Toyota inapanga kuacha kutengeneza gari lake aina ya Corolla Fielder kuanzia keshokutwa Alhamisi, pamoja na aina zingine mbili kwenye viwanda vilivyopo katika mikoa ya Miyagi na Iwate.

Kampuni ya Mazda inajiandaa kusitisha utengenezaji wa gari lake aina ya Roadster RF na gari lingine kwenye viwanda vilivyopo katika mikoa ya Hiroshima na Yamaguchi.

Wakati huo huo, kampuni ya Yamaha imebainika kufanya vipimo vya kelele kwenye aina tatu za pikipiki chini ya hali zisizofaa. Kampuni hiyo imesitisha usafirishaji wa aina moja ya YZF-R1.

Wasiwasi unaongezeka kuhusu athari ambazo kashfa hizi zitakuwa nazo kwa chumi za maeneo na wabia wa biashsara.