Serikali ya Japani yaanza ukaguzi katika makao makuu ya Toyota

Maafisa wa serikali wanafanya ukaguzi katika makao makuu ya kampuni ya kutengeneza magari ya Toyota Motor mkoani Aichi katikati mwa Japani.

Ukaguzi huo unafuatia kukiri kwa kampuni hiyo na kampuni zingine nne kuwa zilighushi majaribio ya utendaji kazi ili kupata uthibitisho wa bidhaa zao.

Ukaguzi wa wizara ya uchukuzi ulioanzishwa tarehe nne Juni unatokana na sheria ya magari barabarani. Inajaribu kubaini ni data zipi za majaribio zilighushiwa na sheria husika za kampuni hiyo.

Kampuni ya Toyota imethibitisha kuwa ilighushi data za majaribio ya magari kuigiza kugonga waenda kwa miguu. Majaribio hayo yalihusu aina tatu za magari ambayo yanaendelea kutengenezwa.

Aidha kampuni hiyo ilithibitisha kuwa ilighushi uundaji wa magari yanayotumika katika majaribio ya magari kugongana. Hii ilihusisha aina nne za magari ambazo haziendelei kuzalishwa.

Kampuni zingine ambazo zilikiri makosa ni Mazda, Yamaha, Honda na Suzuki. Wizara inasema itafanya ukaguzi katika kampuni hizo pia.

Ujumbe wa mhariri: Katika makala yetu ya awali, tuliandika, "Toyota imethibitisha kwamba ilighushi data inayohusiana na majeraha ya kichwa waliopata watembea kwa miguu kwenye ajali." Tumebadilisha sentensi ili kuweka wazi kwamba data ilitokana na majaribio ya maigizo na sio ajali halisi.