India kuhesabu kura zilizopigwa kwenye uchaguzi uliodumu wiki kadhaa

India inajiandaa kuanza kuhesabu kura zilizopigwa katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliodumu wiki kadhaa. Waangalizi wanasubiri kuona iwapo chama tawala kinachoongozwa na Waziri Mkuu Narendra Modi kitajihakikishia muhula wa tatu mfululizo mamlakani.

Mwezi Aprili mwaka huu, wapiga kura nchini India walianza kupiga kura kuwachagua wawakilishi katika maeneo 543 ya uchaguzi kote nchini humo. Chaguzi zilifanyika kwa awamu saba.

Zoezi la kuhesabu kura litaanza saa mbili asubuhi leo Jumanne kwa saa za nchi hiyo.

Wakati wa kampeni ya uchaguzi, Modi alisafiri kote nchini India na kutoa hotuba zaidi ya 200.

Aliwasihi wapiga kura kukiunga mkono chama chake cha Bharatiya Janata, BJP. Alisisitiza kwamba India imefikia ukuaji mkubwa wa kiuchumi chini ya serikali yake.

Vyama vya upinzani vinasema watu wengi wameshindwa kunufaika na maendeleo ya kiuchumi ya nchi hiyo, na kwamba mapengo kati ya matajiri na maskini yanaongezeka.

Vyama hivyo aidha vilikosoa sera za serikali. Vinasema sera hizo zinawapendelea Wahindu ambao ni wengi na kuchochea mashindano ya kidini kati ya Wahindu na Waislamu walio wachache.

Vyombo vya habari nchini India vinasema kura za maoni zinaonyesha kundi linalotawala, kuzungukia chama cha BJP cha Modi, linaelekea kushinda viti vingi ambavyo linahitaji ili kusalia mamlakani.