Nagasaki yaamua kutomwalika balozi wa Israel kwenye hafla ya kila mwaka ya amani

Meya wa jiji la Nagasaki Suzuki Shiro anasema ameamua kutomwalika balozi wa Israel nchini Japani katika hafla ya kila mwaka ya kuadhimisha kudondoshwa kwa bomu la atomiki la Marekani jijini humo.

Suzuki alielezea uamuzi wake kwenye mkutano na wanahabari jana Jumatatu.

Alisema alifanya uamuzi mgumu kwa kuzingatia hali mbaya ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, pamoja na namna janga hilo linavyoangaziwa na watu kote duniani.

Pia alisema kwamba badala yake atatuma barua kwa balozi wa Israel ya kutoa wito wa machafuko kusitishwa mara moja huko Gaza.

Meya huyo alisema jiji hilo litatuma barua ya mwaliko kwa mjumbe wa Palestina nchini Japani kama kawaida.

Jiji la Nagasaki litatuma barua ya mwaliko kwa jumla ya mataifa na maeneo 154. Maafisa wanasema Urusi, ambayo inaendelea na uvamizi wake nchini Ukraine, na mshirika wake Belarus pia zimeachwa nje kwenye orodha ya mwaliko ya jiji hilo.