Spika wa bunge la Georgia atia saini kuwa sheria mswada tatanishi wa ‘ushawishi wa kigeni’

Spika wa bunge la Georgia Shalva Papuashvili ametia saini kuwa sheria mswada tatanishi wa “ushawishi wa kigeni”, ambao wataalam wanasema unaweza kuwa na athari kwa ombi la nchi hiyo la kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Papuashvili jana Jumatatu alitia saini mswada huo kuwa sheria baada ya bunge Jumanne iliyopita kuuidhinisha kwa mara ya pili katika juhudi za kukabiliana na kura ya turufu ya Rais Salome Zourabichvili.

Mswada huo - - ambao utahitaji mashirika yanayopokea asilimia 20 ya ufadhili wao kutoka nje ya nchi kujisajili kama “mawakala wa ushawishi wa kigeni” - - umezua maandamano makubwa yaliyodumu kwa majuma kadhaa katika mji mkuu wa Tbilisi. Wabunge wa upinzani wanaupinga mswada huo wakisema unafanana na sheria ya Urusi inayoweka ukomo wa shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali na vyombo vya habari visivyoipendelea serikali.

Georgia, ambayo imekuwa ikisaka uanachama wa EU, ilipewa hadhi ya mgombea mwezi Disemba mwaka jana.

EU imesema sheria hiyo iliyopitishwa na bunge la Georgia “inaenda kinyume cha kanuni na maadili ya msingi ya EU” na kwamba “itaathiri vibaya njia ya Georgia kujiunga na umoja huo.”

Chama tawala kilichoongoza mchakato wa kupitisha sheria hiyo kitaangaziwa mno wakati wa chaguzi za bunge zilizopangwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.