TEPCO Power Grid: Umeme ulikatika kwa muda eneo la Kanto Jumapili

Kampuni ya umeme ya TEPCO Power Grid inasema kupungua kwa muda kwa volteji kulitokea sehemu nyingi katika eneo la Kanto jana Jumapili alasiri kutokana na athari za radi pamoja na hali zingine za hewa.

Kampuni hiyo imetangaza kuwa hali kama vile umeme kukatika kwa muda ilitokea majira ya saa 9:30 jioni katika mikoa ya Tokyo, Kanagawa, Chiba, Saitama, Ibaraki na Gunma.

Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya Japani inasema kuwa mvua kubwa ilinyesha katika maeneo ya Tokai na Kanto jana Jumapili. Maafisa wanasema hali za angahewa si thabiti zaidi kwa sababu ya hewa ya baridi kali inayoelekea mashariki na kaskazini mwa Japani pamoja na hewa yenye unyevunyevu inayoelekea kwenye mfumo wa mgandamizo mdogo wa hewa katika Bahari ya Japani.

Maafisa wa hali ya hewa wanasema hali za angahewa zisizokuwa thabiti zinatarajiwa kuendelea hadi leo Jumatatu usiku katika maeneo ya Kantokoshin na Tohoku.

Wanatoa wito kwa watu kuchukua tahadhari dhidi ya radi, vimbunga na upepo mkali, mvua za mawe na mvua kubwa.