Miaka 35 baada ya tukio la Uwanja wa Tiananmen, sauti za familia za wafiwa zakandamizwa

Inatimia miaka 35 leo Jumanne tangu kutokea kwa ukandamizaji uliosababisha vifo wa China dhidi ya waandamanaji wanaounga mkono demokrasia katika Uwanja wa Tiananmen jijini Beijing.

Mamlaka zimeweka udhibiti mkali chini ya utawala wa Rais Xi Jinping. Zimekandamiza kabisa miito kutoka kwa familia za wafiwa ya kutafuta ukweli wa tukio hilo.

Mnamo Juni 4 mwaka 1989, vikosi vya China viliwafyatulia risasi wanafunzi na wengineo waliojikusanya ndani na karibu na uwanja huo kudai demokrasia. Serikali ya China inasema watu 319 walifariki, lakini baadhi ya watu wanasema idadi hiyo ni kubwa zaidi.

Kundi la jamaa wa waathiriwa linaloitwa “Mama wa Tiananmen” liliweka taarifa kwenye tovuti yake mwezi uliopita iliyosainiwa na watu 114.

Taarifa hiyo ilitoa wito kwa serikali kuweka hadharani idadi ya waathiriwa na majina yao, kuwalipa fidia waathiriwa na familia zao, na kutafuta uwajibikaji wa kisheria kwa tukio hilo.

Umma nchini China hauwezi ukasoma taarifa hiyo ya mtandaoni kwani ufikiaji wake umezuiwa nchini humo.

Kujadili tukio hilo hadharani kunachukuliwa kuwa mwiko nchini China. Serikali inashikilia kuwa tukio hilo lilikuwa ni “machafuko” na ilifanya uamuzi sahihi.