Chama cha ANC Afrika Kusini chapoteza viti vingi bungeni kwa mara ya kwanza

Chama tawala cha African National Congress, ANC nchini Afrika Kusini ambacho kimekuwa madarakani kwa kipindi cha miongo mitatu iliyopita kwa mara ya kwanza kimepoteza viti vingi katika bunge la taifa.

Tume ya uchaguzi nchini humo jana Jumapili ilitangaza matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Jumatano wiki iliyopita.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa chama cha ANC kilishinda viti 159 kati ya 400 katika bunge la taifa. Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa chama hicho kushindwa kupata viti vingi katika uchaguzi wa kitaifa.

Mnamo mwaka wa 1994, chama cha ANC kilishinda uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini Afrika Kusini ambapo raia wa asili zote walikubaliwa kupiga kura. Nelson Mandela alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza mweusi wa nchi hiyo wakati wa uchaguzi huo.

Lakini uungwaji mkono wa chama hicho umepungua wakati kukiwa na hali inayoongezeka ya umma kuvunjika moyo kufuatia ufisadi uliokithiri, kudorora kwa uchumi na kuzorota kwa usalama.

ANC inatarajiwa kuanza majadiliano ya kuunda serikali ya muungano na vyama vingine, kikiwemo Democratic Alliance, DA kinachoongozwa na wazungu kilichoibuka cha pili kwa kushinda viti vingi. Kingine ni chama kilichoibuka cha tatu kinachoongozwa na rais wa zamani Jacob Zuma aliyeondoka ANC.