Hakuna dosari zilizoripotiwa kwenye mitambo miwili ya umeme wa nyuklia kufuatia tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.0

Mamlaka ya Udhibiti wa Nyuklia nchini Japani inasema hakuna dosari zilizoripotiwa kwenye mitambo miwili ya umeme wa nyuklia kando na pwani ya Bahari ya Japani kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea leo Jumatatu asubuhi.

Tetemeko lenye ukubwa wa 4 kwenye kipimo cha matetemeko ya ardhi cha Japani kinachoanzia sifuri hadi saba lilirekodiwa kwenye mtambo wa umeme wa nyuklia wa Kashiwazaki-Kariwa mkoani Niigata.

Tetemeko hilo lilikuwa la ukubwa wa 3 kwenye mtambo wa umeme wa nyuklia wa Shika mkoani Ishikawa.

Mamlaka hiyo inasema viwango vya mionzi bado havijabadilika kwenye mitambo hiyo.

Vinu vyote kwenye mitambo hiyo miwili havijafanya kazi kwa muda mrefu.