Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.0 katika kipimo cha Richter laukumba mkoa wa Ishikawa

Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini Japani inasema tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.0 katika kipimo cha Richter limeukumba mkoa wa Ishikawa. Mamlaka zinasema hakuna tishio la tsunami.

Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa inasema tetemeko hilo lilitokea majira ya saa 12:31 asubuhi leo Jumatatu huku kitovu chake kikikadiriwa kuwa na kina cha kilomita 14.

Imeongeza kuwa miji ya Wajima na Suzu, yote inayopatikana mkoani humo, ilikumbwa na matetemeko yenye ukubwa wa kiwango cha 5 kwenye kipimo cha matetemeko cha Japani kinachoanzia sifuri hadi saba.

Mamlaka hiyo inasema tetemeko hilo pia lilisababisha matetemeko yenye ukubwa wa kiwango cha 5 mjini Noto, na ukubwa wa kiwango cha 4 katika jiji la Nanao, mjini Anamizu mkoani humo na katika baadhi ya manispaa mkoani Niigata.

Shirika la East Japani Railway linasema huduma za usafiri wa treni za mwendokasi za Hokuriku Shinkansen na Joetsu Shinkansen zilisitishwa kwa muda kutokana na kukatika kwa umeme. Huduma hizo zote zilirejea saa 12:50 asubuhi.