OPEC+ yakubali kuongeza muda wa kupunguza uzalishaji wa mafuta kwa mwaka mmoja

Kundi la mataifa yanayozalisha mafuta kwa wingi, linalojulikana kama OPEC Plus, limekubali kuongeza mpangokazi wake wa sasa wa kupunguza uzalishaji kwa mwaka mmoja hadi mwisho wa mwaka 2025.

Umoja wa Nchi Zinazouza Mafuta Nje ya Nchi na nchi zingine zinazozalisha mafuta kwa wingi kama vile Urusi zilifanya mkutano wa mawaziri kwa njia ya mtandao jana Jumapili.

Katika taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo, kundi hilo lilisema limeridhia kuongeza muda uliopo wa kupunguza uzalishaji ambao ulipaswa kumalizika mwishoni mwa mwaka huu. Hii inamaanisha kuwa kupunguzwa kwa uzalishaji wa mapipa milioni 3.66 ya mafuta kwa siku kutaendelea hadi mwaka 2025.

Nchi nane wanachama, ikiwa ni pamoja na Saudi Arabia na Iraq, pia kwa hiari zitaongeza muda wa kupunguza uzalishaji wa mapipa milioni 2.2 ya mafuta kwa siku kwa miezi mitatu hadi mwisho wa mwezi Septemba.

Zinasema taratibu zitaondoa kwa awamu upunguzaji wa uzalishaji kuanzia mwezi Oktoba huku zikifuatilia mienendo katika soko la mafuta ghafi.