Korea Kaskazini yasema itaacha kwa muda kutuma maputo yaliyojazwa taka

Korea Kaskazini imesema kwamba itasitisha kwa muda kutuma maputo yaliyojazwa taka nchini Korea Kusini. Lakini pia imetishia kurejelea operesheni hiyo ikiwa upande wa Korea Kusini utatuma vipeperushi zaidi vya kupinga Korea Kaskazini nchini Korea Kaskazini.

Korea Kaskazini imekuwa ikituma maputo yaliyojazwa taka tangu Jumanne wiki iliyopita. Inaonekana ilikuwa inalipiza kisasi dhidi ya vitendo vya baadhi ya wanaharakati nchini Korea Kusini. Wanaharakati hao walituma maputo yenye vipeperushi vya kukosoa uongozi wa Korea Kaskazini nchini Korea Kaskazini.

Ofisi ya rais wa Korea Kusini ilikuwa imetoa onyo jana Jumapili kwamba itachukua hatua "zisizovumilika" dhidi ya Korea Kaskazini, ikiwa haitaacha kutuma maputo yaliyojazwa taka.

Baadaye jana Jumapili, Makamu wa Waziri wa Ulinzi wa Korea Kaskazini Kim Kang Il alitangaza kwamba operesheni ya puto ilikuwa inasitishwa kwa muda. Alidai kuwa Korea Kaskazini ilituma tani 15 za taka za karatasi.

Shirika la habari la serikali ya Korea Kaskazini la Korean Central News lilirusha taarifa ya Kim. Alisema Korea kaskazini imewapa Wakorea Kusini uzoefu kamili wa jinsi inavyochukiza na ilivyo kazi ngumu kukusanya taka za karatasi zilizotawanyika.