Korea Kaskazini yatuma maputo ya taka zaidi kuelekea Korea Kusini

Jeshi la Korea Kusini linasema kwamba Korea Kaskazini imerusha tena maputo yaliyobeba takataka kuelekea Korea Kusini.

Wakuu wa Majeshi ya Korea Kusini walisema kwamba urushaji huo ulianza majira ya saa mbili usiku jana Jumamosi.

Walisema kwamba takribani maputo 90 kama hayo yaliyopatikana, yaliyodondosha vipisi vya sigara na taka za karatasi katika mji mkuu Seoul na maeneo ya jirani na Jimbo la Gyeonggi.

Jeshi linawashauri watu kuwa makini na vifaa vinavyodondoka na kulitaarifu jeshi ama polisi iwapo watabaini vitu wanavyovitilia shaka.

Korea Kaskazini ilirusha maputo kama hayo yapatayo 260 kuelekea maeneo mbalimbali ya Korea Kusini ikiwemo Seoul siku kadhaa zilizopita.

Waziri wa Ulinzi wa Korea Kusini Shin Won-sik jana Jumamosi aliilaani Korea Kaskazini akikiita kitendo hicho kuwa kibaya katika hotuba alioitoa kwenye Mkutano wa Usalama wa Viongozi Wakuu wa Asia nchini Singapore.

Shirika la habari la Korea Kusini, Yonhap liliripoti kwamba Korea Kaskazini ilituma ishara za mgongano za GPS kwenye Bahari ya Njano magharibi mwa Rasi ya Korea kwa siku nne mfululizo hadi jana Jumamosi.

Korea Kusini inasema inaviangazia vitendo vya hivi karibuni vya kichokozi vya Korea Kaskazini kwa umakini mkubwa.