Upigaji kura katika uchaguzi wa India wamalizika, muungano wa Modi watabiriwa kushinda

Upigaji kura wote katika uchaguzi mkuu nchini India umemalizika jana Jumamosi. Vyombo vya habari nchini humo vimetoa matokeo ya awali yakionesha muungano wa vyama vya Waziri Mkuu Narendra Modi ukionekana kuelekea kushinda viti vingi bungeni vinavyohitajika kuendelea kumuweka madarakani.

Duru ya mwisho ya duru saba za uchaguzi, ambao ni uchaguzi mkubwa zaidi duniani wenye watu wanaostahili kupiga kura takribani bilioni moja, ilimalizika jana Jumamosi. Kura zilipigwa katika majimbo 543 ya uchaguzi.

Modi anaongoza serikali ya Chama cha Bharatiya Janata ama BJP na anatafuta muhula wa tatu kama waziri mkuu. Chama hicho kilishinda viti vingi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2019, na muungano huo wa vyama tawala ulipata takribani theluthi mbili ya viti vyote.

Kura za maoni za vyombo vya habari zinatabiri kuwa kasi hiyo itaendelea kipindi hiki pia.

Vyama vya upinzani vinalalamika kuwa matokeo ya kura za maoni hayaakisi kwa usahihi kura halisia.

Wakati wa kampeni za uchaguzi, muungano wa vyama tawala uliangazia umaarufu wa Modi katika kuongeza uungwaji mkono. Muungano huo ulisisitiza kuwa uongozi wake imara umeipelekea nchi kukua kiuchumi.

Vyama vya upinzani vililenga kushinda ukosoaji wa wapiga kura kwa Modi kwa kusema ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana na tofauti za kiuchumi vilianza kuongezeka chini ya utawala wake.

Zoezi la kuhesabu kura litafanyika kote nchini humo kesho kutwa Jumanne.