Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump aahidi kukata rufaa

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump anasema yupo tayari kupambana juu ya hukumu yake ya kupatikana na hatia. Alifanya mkutano na wanahabari kwenye ukumbi wa Trump Tower jijini New York nchini Marekani jana Ijumaa, siku moja baada ya kupatwa na hatia ya kupotosha rekodi za kibiashara kabla ya uchaguzi wa mwaka 2016. Alisema anapanga kukata rufaa ya uamuzi, aliyoielezea kama ni “kashfa.”

Trump amekuwa mtu wa kwanza aliyewahi kuhudumu kama rais wa Marekani kushitakiwa kwa uhalifu. Alikutwa na hatia kwenye mashitaka yote ya uhalifu katika kesi, iliyojikita katika jaribio lake la kuficha malipo kwa mchezaji nyota wa filamu za watu wazima ili kumzuia asitoe taarifa kuhusu mahusiano yao ya kimapenzi.

Alitumia mkutano huo wa wanahabari kudai kwamba kesi hiyo ilichochewa kisiasa. Alisema yupo chini ya agizo la jaji, na kwamba hakuna mgombea wa urais aliyewahi kuwa chini ya maagizo ya jaji hapo kabla. Aliongeza kwamba kesi hiyo “haikuwa ya haki” na “yote yamefanywa” na Rais Joe Biden “na watu wake.”

Hukumu imepangwa kusomwa Julai 11. Trump anakabiliwa na hukumu ya kuanzia kuwa chini ya uangalizi hadi kifungo cha miaka minne jela kwa kila moja ya makosa 34. Ana siku 30 za kukata rufaa baada ya hukumu hiyo.