Majadiliano ya kusitisha mapigano ya Israel na Hamas yakwama huku raia wa Gaza wakisubiri msaada

Vikosi vya Israel vilisema jana Ijumaa kwamba wanaendelea kupiga hatua katika mapambano dhidi ya kundi la Hamas. Waliteka eneo muhimu kando ya mpaka wa Gaza na Misri, pamoja na kusonga mbele kuelekea katikati ya eneo la Rafah. Majadiliano ya kusitisha mapigano yamekwama, na pande zote zinatupiana lawama kwa kukosekana mafanikio ya majadiliano.

Viongozi wa kundi la Hamas walisema katika taarifa ya juzi Alhamisi kuwa wapo tayari kwa ajili ya “makubaliano kamili,” ikiwemo kuachiwa mateka waliokamatwa mwezi Oktoba, iwapo Israel itasitisha mashambulizi. Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Israel, maafisa hapo walisema hawatakubali kuhitimisha vita kwa mabadilishano ya mateka.

Mapigano katika eneo la Rafah yamesababisha kupungua kwa kiasi kikubwa misaada inayoingia Ukanda wa Gaza. Maafisa wa Israel walisema jana Ijumaa kwamba bidhaa katika malori yanayokadiriwa kufikia 600 zinasubiri kuchukuliwa kutoka upande wa Gaza wa mpaka wa Kerem Shalom.

Hata hivyo, wafanyakazi wa misaada wanasema kuna mambo mengi zaidi yanayohitajika kufanyika.