Nchi za Ulaya zatoa msaada zaidi wa kijeshi kwa Ukraine

Nchi za Ulaya zinaongeza msaada wao wa kijeshi kwa Ukraine, huku vikosi vya Urusi vikiongeza mashambulizi yao kwenye maeneo ya mashariki mwa Ukraine.

Uswidi ilisema Jumatano wiki hii kwamba itaongeza msaada wa ziada wa yuro bilioni 1.16 ama takribani dola bilioni 1.26, kukuza uwezo wa ulinzi wa Ukraine.

Msaada huo mkubwa zaidi kuwahi kutolewa na Uswidi unajumuisha ndege za upelelezi na udhibiti wa anga zenye uwezo wa kutambua malengo ya mbali kwenye anga ama baharini.

Gazeti la The Guardian la Uingereza liliripoti kwamba hii itakuwa ni “mara ya kwanza kwa Ukraine kuwa na uwezo kama huo tangu kuvunjika kwa Umoja wa Kisovieti.”

Lilibainisha ndege hizo zinaweza kutuma taarifa kwa ndege za kivita za F-16 ambazo Ukraine itazipokea kutoka kwa washirika wake.

Vyombo vya habari vya Ukraine pia vinasisitiza umuhimu wa msaada huo, vikisema jeshi la nchi hiyo hadi sasa limekuwa likifuatilia shughuli za anga kwa kutumia mifumo ya rada ya ardhini.

Waziiri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius Alhamisi wiki hii alitangaza msaada mpya wa kijeshi kwa Ukraine wenye thamani ya karibu dola milioni 540.

Unajumuisha makombora ya ulinzi wa anga, droni kwa ajili ya upepelezi juu ya Bahari Nyeusi, na vipuri kwa ajili ya mifumo ya makombora ambayo tayari yametolewa.