Mawaziri wa ulinzi wa Japani na China wakubaliana kukuza mazungumzo

Waziri wa Ulinzi wa Japani Kihara Minoru amewasilisha wasiwasi wa nchi yake kuhusiana na shughuli China katika Bahari ya China Mashariki kwenye mkutano wake wa kwanza na waziri wa ulinzi wa China, Dong Jun uliofanyika nchini Singapore jana Jumamosi.

Mawaziri hao walikubaliana kuendeleza namba ya simu ya dharura iliyoanzishwa mwaka jana kati ya mamlaka zao za ulinzi, na kukuza mazungumzo pamoja na mabadilishano.

Kihara alifungua mkutano wa kwanza wa mawaziri wa ulinzi kati ya nchi hizo mbili uliofanyika baada ya kupita mwaka kwa kusema wasiwasi mwingi wa kiusalama upo kati yao. Aligusia China kuongeza shughuli za kijeshi karibu na eneo la Japani na shughuli za baharini katika Bahari ya China Mashariki, ikiwa ni pamoja na maeneo karibu na Visiwa vya Senkaku Mkoani Okinawa.

Japani inavidhibiti visiwa hivyo vya Senkaku. Serikali ya Japani inadai kuwa visiwa hivyo ni sehemu ya urithi wa maeneo ya nchi hiyo. China na Taiwan zinadai umiliki wa visiwa hivyo.

Kihara alisisitiza umuhimu wa kuendeleza majadiliano kati ya mamlaka za ulinzi za mataifa hayo mawili.

Wakati akifikiria mizozo ya uhuru wa kujitawala kati ya China na Ufilipino, Kihara pia alielezea wasiwasi juu ya hali katika Bahari ya China Kusini, na kusisitiza umuhimu wa amani na uthabiti katika Mlango Bahari wa Taiwan.

Dong alisema mamlaka za ulinzi za mataifa hayo mawili lazima zifanye vizuri kutekeleza sera na vitendo ambavyo mataifa hayo mawili hayavioni kama ni tishio, na kwamba anataka kuendelea kuwasiliana na Kihara.