Mkoa wa Ishikawa unahangaikia kuzuia vifo vinavyotokana na majanga miezi mitano baada ya tetemeko la ardhi

Mamlaka katika Mkoa wa Ishikawa zinaendelea kukabiliwa na changamoto ya kuzuia vifo vinavyotokana na majanga na kutengwa kijamii kwa watu katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko kubwa la ardhi la Siku ya Mwaka Mpya katikati mwa Japani.

Leo Jumamosi inatimia miezi mitano tangu tetemeko la ardhi lilipoikumba Rasi ya Noto. Maafisa wa mkoa wa Ishikawa wanasema watu 260 wamethibitika kufariki katika mkoa huo huku wengine watatu hawajulikani mahala walipo.

Miongoni mwa waathirika, 30 walifariki kutokana na sababu zinazohusiana na janga hilo, kama vile dhiki na uchovu, huku wakiishi mbali na makazi yao. Idadi ya vifo kama hivyo inaweza ikaongezeka zaidi.

Juhudi zinafanyika kujenga makazi ya muda kwenye jamii zilizoathirika. Zaidi ya nyumba 4,400 zimekwishajengwa hadi sasa, sawa na takribani asilimia 70 ya idadi inayokadiriwa na mkoa kuwa ni muhimu.

Kadiri wahamaji wengi zaidi wakihamia kwenye nyumba za muda, mamlaka za mkoa wa Ishikawa zinakabiliana na hatari ya vifo vinavyohusiana na janga hilo na kutengwa.

Zaidi ya watu 3,000 bado wanaishi kwenye vituo vya uhamaji, wakisubiri kuhamia kwenye makazi ambapo wataishi kwa utulivu wa akili.