Serikali ya Japani yaahidi dola milioni 330 kwa ajili ya ujenzi wa Rasi ya Noto iliyokumbwa na tetemeko la ardhi

Serikali ya Japani imeamua kutoa mamia ya mamilioni ya dola kwa Mkoa wa Ishikawa ili kusaidia juhudi za ujenzi mpya, miezi mitano baada ya tetemeko kubwa la ardhi kuipiga Rasi ya Noto iliyopo katikati mwa Japani siku ya Mwaka Mpya.

Wakulima katika mji wa Wajima wanapanda miche ya mpunga katika mashamba ya mpunga. Kufikia katikati ya mwezi wa Mei, walikuwa wamemaliza kukarabati njia za umwagiliaji maji zilizoharibiwa na tetemeko hilo, lakini mkulima Ura Tsuneo anasema bado changamoto zimesalia.

Ura ilimbidi asawazishe mashamba yake ambayo yaliharibiwa na tetemeko hilo, kwa hivyo anatarajia kupanda miche ya mpunga kutachukua takribani mwezi mmoja zaidi ya kawaida.

Serikali kuu ya nchi hiyo ilifanya uamuzi wake jana Ijumaa katika mkutano wa kikosikazi kuhusu maafa hayo. Takribani dola milioni 330 zitaingia katika hazina ya ujenzi mpya itakayoanzishwa na Mkoa wa Ishikawa, na pesa zitakazopatikana kutokana na mapato ya kodi zilizotengwa kwa ajili ya mahitaji maalum ya serikali za mitaa.

Kiasi hicho ni kikubwa kwa msaada wa serikali baada ya tetemeko la ardhi la Kumamoto la mwaka 2016, ambacho kilifikia takribani dola milioni 325.